
KUTOKA CHUMBA CHA HABARI
Kiongozi wa upinzani nchini Myanmar, Aung San Suu Kyi ameachiwa huru leo na uongozi wa kijeshi wa nchi hiyo.
Uongozi wa kijeshi nchini Myanmar umemuachia huru kiongozi wa upinzani nchini humo, Aung San Suu Kyi. Magari maalum leo yaliwasili katika nyumba ya kiongozi huyo iliyoko pembezoni mwa ziwa na polisi waliondoa vizuizi pamoja na senyenge.
Suu Kyi aliusalimia umati wa wafuasi wake wapatao 1,000 ambao walikuwa wamekusanyika katika lango la kuingilia kwenye nyumba hiyo. Mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel, ametumikia kifungo cha nyumbani kwa takriban miaka 21.
Kitendo cha kuachiwa kwa mtetezi huyo wa demokrasia kimepongezwa na viongozi mbalimbali wa Ulaya, Marekani na Jumuiya ya mataifa ya Kusini-Mashariki mwa Asia-ASEAN.
Kifungo hicho cha nyumbani dhidi ya Suu Kyi kimemalizika ikiwa ni wiki moja baada ya vyama vinavyoungwa mkono na uongozi wa kijeshi wa Myanmar kushinda katika uchaguzi ambao mataifa ya Magharibi yameuelezea kama wa uzandiki.
Imeandikwa na: Grace Kabogo (AFP, DPA)
No comments:
Post a Comment