Na Johnson Jabir
ZAIDI ya vijana 100 wa mikoa ya Mbeya, Dar es Salaam na Visiwani Zanzibar wameungana na kuunda Umoja utakaowasaidia kudai haki za vijana hapa nchini kutokana na vijana wengi kutotambua wajibu wao katika jamii.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa Kanda za Dar es Salaam na Mbeya, walisema umoja huo kwa sasa upo katika hatua za mwisho za usajili ambao utajikita zaidi katika masuala ya vijana walio na umri wa miaka 15 hadi 35.
Waliongeza kuwa umoja huo utajulikana kwa jina la MUHUVITA ambao utapigania vijana kujitambua, vilevile utajishughulisha na utunzaji wa Mazingira, utoaji wa elimu juu za dawa za kulevya kwani kundi kubwa linalotumia ni vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa la Tanzania.
“tangu tumepata uhuru hapa nchini mwaka 1961 hatujawahi kuona umoja wa vijana wenye madhumuni kama haya tulionayo ukianzishwa, na hata msajili mwenyewe ameshangaa na kusema hajawahi kuona vijana wakija na kusajili muungano wowote”.
Licha ya kujikita zaidi katika masuala ya vijana wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 35 watajishughulisha pia na kupigania unyanyapaa wa watoto walio na umri chini ya miaka 15 hasa ukizingatia vitendo vya kikatili kwa watoto hao vimekuwa vikiongezeka siku baada ya siku, pia wakitoa elimu hiyo kwa wahusika kutasababisha watoto hao kukua vizuri huku wakitambua haki zao za msingi.
Hata hivyo wamejipanga kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza na kusema madhumuni hasa ni kuirudisha nchi ya Tanzania katika hali yake kwani uzalendo umeonekana kupungua hususani kwa vijana ambao wengi wao wamekuwa wakitorokea ng’ambo kwa kudhani kuwa maisha bora yanapatikana huko na kuacha nafasi nzuri zilizopo bila kujali kwamba pato la taifa linapungua.
“vijana wengi wamekimbilia ng’ambo wakidhani watapata maendeleo lakini hakuna fursa nzuri kama zilizopo hapa Tanzania na wengine kwa kwenda huko wamepoteza maisha yao kitu ambacho ni hatari kwani kijana mmoja akipotea, nguvu kazi ya taifa inashuka kwa asilimia 90 ya uzalishaji”.
Kwa kuanza wameganyawa kanda tatu ambazo ni Dar es Salaam, Mbeya na Zanzibar huku wakitegemea kupanua zaidi matawi nchi nzima.
No comments:
Post a Comment