Na Abraham Mbugula
WANANCHI wa Jimbo la Mbeya Vijijini wamemtaja mgombea ubunge kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Sambwee Mwalyego Shitambala, kuwa ni tumaini jipya kwa maendeleo jimboni humo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi wa kitongoji cha Mbalizi ambako kulifanyika uzinduzi wa kampeni za CHADEMA, walisema kuwa wanamtegemea Shitambala kuwa mwakilishi wao mzuri bungeni kutokana na sera zake alizozitoa na jinsi wanavyomfahamu.
Akizindua kampeni hizo zilizofanyika maeneo ya Tarafani Mbalizi Shitambala alisema kuwa anawataka watu wa Mbeya vijijini wawe wabunge wenyewe, ndipo wamtume yeye akawawakilishe bungeni.
Shitambala alisema kuwa katika kipindi chake cha uongozi atahakikisha anashughulikia kikamilifu suala la mbolea inayotolewa na serikali kwani watu wa Mbeya vijijini wanategemea zaidi kilimo.
Pia alisema kwamba atashughulikia suala la Elimu na kwamba atajitahidi kuwawezesha wanafunzi wanaoshindwa kufanya vizuri darasani kwa namna yoyote ile hata kama sio kuingia darasani ili mradi wasikae nyumbani na kuishia kushinda vijiweni.
Aidha Shitambala aliwataja wagombea udiwani kupitia chama hicho cha CHADEMA kuwa ni Difasi Mwakisale kwa kata ya Nsalala na Elia Mkono wa kata ya Utengule-Usongwe Mbeya vijijini.
No comments:
Post a Comment