Mbeya Institute Of Journalism (MIJO) inakukaribisha katika mwaka wa masomo wa Februari hadi Desemba 2010



Serikali ya Wanafunzi ya Chuo (SOMIJO) inakukaribisha kwa moyo mkunjufu katika tasnia hii ya Uandishi wa Habari zilizojawa na ukweli zenye kuleta maendeleo kwa mwananchi husika na taifa kwa ujumla.

Tuesday, August 17, 2010

WAWILI WAFA MBEYA

Na Johnson Jabir

WATU wawili wamefariki dunia juzi katika matukio mawili tofauti na wengine kujeruhiwa vibaya mkoani Mbeya.


Katika tukio la kwanza mkazi wa Ikuti-Iyunga Jijini Mbeya aliyefahamika kwa jina moja la Hassan anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 hadi 35, alifariki wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mbeya baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa marehemu akiwa na wenzake wawili walivunja na kuiba masanduku ya chupa za bia tupu katika kiwanda cha kutengeneza bia (TBL) majira ya saa 5:00 usiku, ambapo thamani ya masunduku haikujulikana mara moja.

Waliojeruhiwa katika tukio hilo, Amoni Damiani(31) mkazi wa Inyara-Iyunga na Nestory Mgaya(22) mkazi wa Nzovwe Jijini humo, ambao wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa huku wakiwa chini ya Ulinzi wa Polisi na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali hiyo.

Katika tukio jingine Mpanda baiskeli mkazi wa kijiji cha Lunwa, wilayani Mbarali aliyefahamika kwa jina la Fabian Mbikise(23) alikufa papo hapo baada ya kugongwa na gari lenye namba za usajili T 666 BCR, basi aina ya Yutong majira ya saa 1:30 usiku lililokuwa likiendeshwa na Mfaume Hamad katika barabara ya Mbeya-Iringa.

Kufuatia tukio hilo dereva wa basi hilo alikimbia na kulitelekeza basi hilo ambalo hata hivyo liliendeshwa na dereva wa pili ambaye hakufahamika mara moja na kufikishwa katika kituo cha polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Advocate Nyombi amethibitisha kutokea kwa matukio hayo na kuwataka wananchi kutojichukulia sheria mkononi na madereva kuwa waangalifu wawapo na barabarani ili kuleta usalama kwa walio ndani na nje ya vyombo vya usafiri.

No comments:

Post a Comment